Sunday, June 9, 2013

HOJA ZA MWALIMU NYERERE KUPINGA SERIKALI TATU TANZANIA

Nchi mbili zinapoungana na kuwa Nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili: Muungano wa Serikali Moja, au Shirikisho la serikali Tatu. Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake na nchi mpya inayolizaliwa itakuwa ni nchi moja yenye Serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho na itakuwa na serikali ambayo ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki.


Mambo yatakayoshikwa na serikali ya Shirikisho ili yale ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika nchi zilizungana basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi kuwa nchi moja bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.

Nchi za Afrika Mashariki zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Zilikuwa ni Nchi Tatu zenye ushirikiano mkubwa, lakini hazikuwa Nchi Tatu zilizoungana kuwa Nchi Moja yenye muundo wa Shirikisho. Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni Nchi Moja yenye Serikali tatu, Serikali ya Shirikisho, na Serikali mbili za nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.


Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi Moja, tungeweza kufuata mmojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zan­zibar na ukubwa wa Tanganyika. Zan­zibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali Moja

Ungefanya ionekane kama Tangan­yika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tuuhaniwe hata kwa makosa, kwanba tunaanzisha ubeberu mpya!

Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali Moja. Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzi­bar ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha Serikali ya Shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tan­ganyika ndio hasa ungeendesha SerikaIi ya Shirikisho. Kwa hiyo Tan­ganyika ingeendesha Serikali yake ya watu 12, 000, 000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu 12,300,000.

Ni Watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yoyote kati ya hizo ingekuwa ndogo. Gharama ya Serikali ya Tan­ganyika isingekuwa ndogo, (waulizeni Wazanzibari), na wala ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo. Hata bila ya gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tan­ganyika.

Kwa hivyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na SerikaIi yake, itaoekana kuwa imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na Serikali Moja Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute mfumo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha Serikalli mbili zenye uzito unaolingana.

Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa Muungano wa serikali mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazamia hali halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo uliotufaa zaidi.

Mwalimu Nyerere katika Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania

Next Post Previous Post Home

1 comments: