Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ameuliza maswali saba ya
msingi kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaopinga Rasimu ya Katiba
iliyotolewa na Tume yake akitaka wawajibu wananchi ili kutuliza kiu yao.
Jaji Warioba ambaye tangu awasilishe
Rasimu ya Katiba Desemba 30, mwaka jana amegeuka kuwa adui kwa watu
wanaotaka muundo wa serikali mbili, aliuliza maswali hayo jana katika
uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza kuhusu mchakato wa
Katiba.
Akizungumza kwa ukali, Jaji Warioba
alisema: “Kwanza, jibuni kwa nini mnapinga muundo wa Muungano wakati
walioupendekeza ni wananchi?
“Sheria inasema uwepo wa Muungano na
mapendekezo katika rasimu hayasemi Muungano usiwepo. Kumbukeni kuwa
wananchi walitakiwa kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha Muungano.”
Katika swali lake la pili, Warioba
alisema kwa nini Tanganyika imevaa koti la Muungano? Kwa kuwa katika
ukusanyaji wa maoni wananchi walieleza kuwa Serikali ya Muungano ya sasa
siyo ya Muungano, ni ya Tanganyika.
Katika swali la tatu alisema wajumbe hao
wanatakiwa kujibu maelezo ya wananchi ambao waliieleza tume hiyo kuwa
Katiba imevunjwa na madaraka ya rais yamechukuliwa na sasa kuna marais
wawili katika nchi moja.
“Tume inapewa lawama kubwa, wajibuni
wananchi hii tume ilitumwa na nani kukusanya maoni ya wananchi?
Waambieni ilikusanya maoni hayo kwa kutumia sheria ipi zaidi ya ile ya
Mabadiliko ya Katiba?” alisema Jaji Warioba katika swali lake la nne.
Katika swali lake la tano, Warioba
aliwataka wajumbe hao kutoa sababu za kumtuhumu kuwa amependekeza muundo
wa serikali tatu kwa sababu yeye pamoja na (Joseph Butiku) walikuwa
wajumbe wa Tume ya Jaji Kisanga na Jaji Nyalali ambazo nazo
zilipendekeza muundo wa serikali tatu, kitu ambacho alisema si kweli na
hawakuwahi kuwa mjumbe wa tume hizo.
Pia, aliwataka wajumbe hao kujibu swali
la sita, kwa nini hawataki kuzungumzia yaliyomo katika Rasimu ya Katiba
na badala yake wanageuza rasimu hiyo kuwa imeandikwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Katika swali lake la saba, aliwataka
wajumbe kujibu kwa nini wanaishutumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa
imeingiza maoni yake, wakati ilikusanya maoni hayo kwa mujibu wa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba?
Alisema badala ya kujadili hoja za
msingi, wajumbe wa Bunge hilo wamekuwa wakitoa lugha za kejeli na matusi
kwa baadhi ya watu (akiwamo na yeye), kitendo ambacho alisema si sahihi
na kinaweza kuligawa taifa kwa sababu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba
yametokana na maoni ya wananchi.
Katika uzinduzi huo walikuwepo baadhi ya
wajumbe wa Bunge hilo ambao ni Dk Hamisi Kigwangalla aliyemwakilisha
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Julius Mtatiro, Maria Sarungi na
aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole.
Amshukia Lukuvi
Katika maelezo yake, Jaji Warioba
alieleza kushangazwa kwake na wajumbe kulitumia Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), kama mfano wa kuwashawishi Watanzania kukubaliana na
matakwa yao ya kutaka kupinga mfumo wa serikali tatu.
“Nchi hii imekuwa na matatizo ya rushwa
na ufisadi, lakini hakuna hata siku moja mtu amesema jeshi linaweza
kushika madaraka. Leo kwa sababu ya madaraka mnaingiza jeshi na mchakato
wa Katiba katika makundi.”
Licha ya kutomtaja mlengwa, kauli hiyo
ilionekana kumlenga Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu
na Bunge), William Lukuvi ambaye Aprili 13, mwaka huu aliwataka wananchi
kupinga muundo wa serikali tatu, akisema la sivyo jeshi linaweza
kuchukua madaraka.
Akiwa katika Kanisa la Methodist, Jimbo
la Dodoma alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, Lukuvi alisema muundo huo ukipita, nchi itatawaliwa na jeshi kwa
kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.
Kauli kama hiyo pia iliwahi kutolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.
“Msiliingize jeshi katika siasa za
makundi na inakuwa mbaya zaidi kama mkienda katika makanisa na kutoa
kauli za namna hii,” alisema Warioba na kuongeza:
“Umoja wetu, amani na utulivu kwa
kiwango kikubwa mhimili wake ni viongozi wa dini. Wamekuwa wakihubiri
umoja, amani na mshikamano, hivyo tusiingize siasa za makundi kwenye
makanisa na misikiti.”
Jaji Warioba aliwataka wajumbe wa Bunge
hilo kukumbuka wajibu wao wa kuwaunganisha wananchi na kuwataka waachane
na kauli za kejeli, kuudhi na matusi kwani zinaweza kuleta mgawanyiko
na mpasuko nchini.
“Nimekuwa mtumishi wa umma kwa muda
mrefu lakini sijawahi kuona taasisi yenye uzalendo wa hali ya juu kama
JWTZ,” alisema Warioba.
Warioba ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu
na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, kuanzia mwaka 1985 hadi 1990,
alisema: “Katika ziara zangu mikoani nilikuwa nikikutana na wanajeshi na
kunieleza matatizo yao. Licha ya wakati huo serikali za mataifa mengine
zilikuwa zikipinduliwa na jeshi, hapa kwetu ilikuwa tofauti, walikuwa
na uzalendo wa hali ya juu licha ya kuwa hali yetu kiuchumi ilikuwa
mbaya,” alisema.
Alisema wakati huo wanajeshi walikuwa wakivaa sare zilizochakaa na viatu vilivyopasuka, lakini hawakufikiria kuipindua Serikali.
Alisema hata katika vita dhidi ya
Uganda, wanajeshi wa Tanzania walishinda kwa sababu ya uzalendo na siyo
vifaa vya kisasa vya kivita... “Inashangaza kuona watu wanatolea mfano
mmoja tu wa kama wanajeshi wasipolipwa; kwa nini wasiseme mawaziri au
watumishi wa serikali wasipolipwa?”
Alisema kauli hiyo ni sawa na kuwaeleza
wananchi kuwa jeshi ni baya na kama ikipita Katiba isiyoendana na
matakwa ya walio wengi jeshi litachukua nchi.
Alisema wakati Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ikikusanya maoni ya wananchi, wanajeshi na viongozi wa vyombo vya
ulinzi na usalama nchini walijikita zaidi kutoa maoni ya kuimarishwa
kwa ulinzi na usalama na siyo mambo mengine.
“Tatizo ambalo walitueleza ni kuchoshwa
na kitendo cha kupiga mizinga 21 kwa Amri Jeshi Mkuu wakiwa Dar es
Salaam na wakiwa Zanzibar. Walisema kwa nidhamu ya jeshi, Amri Jeshi
Mkuu ni mmoja tu. Nadhani mngewaondolea kero hiyo na si mambo mengine,”
alisisitiza.
Kigwangalla
Kwa upande wake, Dk Kigwangalla alisema
kama tatizo ni Muungano ni vyema suala hilo likarejeshwa upya kwa
wananchi ili watoe maoni yao kwa sababu mchakato huo sasa umehamia
katika muundo wa Muungano pekee.
“Mchakato huu si wa kuifufua Tanganyika
na kuvunja mkataba wa Muungano na siyo wa kubadili muundo wa utawala.
Mambo haya yalihitaji mchakato unaojitegemea,” alisema.
Alisema tume zote zilizotoa mapendekezo
ya Serikali tatu zilikuwa na asilimia ndogo ya watu waliounga mkono kama
ilivyo kwa Tume ya Jaji Warioba.
Source: Udaku special
Thursday, April 24, 2014
MASWALI SABA YA JAJI WARIOBA KWA WAJUMBE WA BUNGE WANAOIPINGA RASIMU YAKE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment