Friday, June 7, 2013

RASIMU YA KATIBA MPYA YALETA HOFU

Dodoma na Dar es Salaam. Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamedai kuwa muungano unaweza kuvunjika kutokana na pendekezo la kuundwa kwa Serikali tatu lililotolewa kwenye rasimu ya Katiba Mpya na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akizungumzia suala hilo, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani na Mbunge wa Iramba Mashariki, Tundu Lissu alisema Tume ya Nyalali na Kisanga ziliona matatizo katika kuunda Serikali tatu kwa kuwa zinaua Muungano, lakini kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, imeuua Muungano.

“Pamoja na kwamba Wazanzibari wengi wamefurahia rasimu ya Katiba kwa kuipa mamlaka Zanzibar na Tanganyika, lakini watambue kuwa itafika hatua na wao watabaguana tu baadaye. “Labda isipite, lakini hili la Serikali tatu likipita, wapo watakaoanza chokochoko kama hizi, Wapemba nao watakuja kudai Jamhuri yao. Watatengana Wapemba na Waunguja ni yaleyale aliyoyaona Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere,” alisema Lissu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mashariki, John Cheyo alihofia kuwepo kwa Serikali tatu, ambapo alibainisha kuwa kama pendekezo hilo litapita, basi Katiba Mpya iwe moja kwa Tanganyika na Zanzibar na mambo muhimu yaingizwe kwenye Katiba ya Shirikisho na iwe katiba moja badala ya kuanza kusaka Katiba Tanganyika na Zanzibar kwa kuwa mambo mengi ni yaleyale kama itaanza kutafutiwa maoni mengine.                

Cheyo aliyewahi kuwania urais kupitia Chama cha UDP, 1995 na 2000 pia alisema kamwe mgombea binafsi wa urais hawezi kushinda nafasi hiyo japokuwa inapangwa kuingizwa kwenye Katiba Mpya. “Kuwepo ndani ya chama kunatengeneza mazingira mengi. unawekewa mazingira ya ushindi, watu wengi wanakuunga mkono kwa sauti moja, sasa ukiwa peke yako, ni kazi kweli kweli pamoja na kwamba itawekwa kwenye mpango, lakini mtu hawezi kushinda,” alisema Cheyo.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mabere Marando alikosoa Rasimu ya Katiba Mpya ibara ya 187, ambayo inampa Rais mamlaka ya kuteua mkurugenzi wa tume ya uchaguzi na mkurugenzi wa usajili wa vyama vya siasa.

Akizungumza jana ofisini kwake Dar es Salaam, Marando ambaye pia ni wakili maarufu nchini alisema kuwa Rais ana hadhi kubwa. Hivyo ni vyema kama rasimu hiyo ingependekeza wakurugenzi hao wachaguliwe na wajumbe wa tume husika ambao wao wanateuliwa na Rais.

“Kuna kiwango cha nafasi za utendaji ambazo Rais anapaswa kuteua, lakini kwa nafasi hizi za wakurugenzi hawa ambao ni watendaji, wajumbe walipaswa kupewa jukumu la kuwachagua kwa kuwaajiri. Pia watumishi wengine wanaotumikia Tume ya Uchaguzi wanapaswa kuwa waajiriwa,” alisema Marando.

 Katika rasimu hiyo Ibara ya 187 kifungu cha 5 inazungumzia kuwa uteuzi wa mkurugenzi wa uchaguzi na msajili wa vyama vya siasa utafanywa na Rais baada ya kuthibitishwa na Bunge na kifungu cha 6 kinaeleza kuwa katika kutekeleza majukumu yao, mkurugenzi wa uchaguzi na msajili wa vyama vya siasa watawajibika kwa Tume Huru ya Uchaguzi.
                              
Tume ya Warioba iliweka hadharani Rasimu ya Katiba Mpya, ikibainisha maeneo mbalimbali ya kufanyia marekebisho kutokana na mawazo ya watu wa kada mbalimbali.

CHANZO:MWANANCHI
 

Next Post Previous Post Home

2 comments: