Saturday, May 18, 2013

SIMBA: MECHI NA YANGA ITASAJILI

*Wasema itafungua mipango yao mipya ya msimu ujao
*Kuwasili leo kwa maji, Yanga kutua na ndege

WAKATI watani wa jadi Simba na Yanga wakitarajia kukutana kesho, katika mchezo wa kukamilisha Ligi Kuu Tanzania Bara, Uongozi wa Klabu ya Simba umesema mchezo wake huo, utafungua mipango mipya ya usajili wa klabu hiyo, kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi.
Timu hizo zinatarajia kupishana njia kuwasili Dar es Salaam, zikitokea katika visiwa vya Zanzibar, Unguja na Pemba walipokuwa wakijiandaa.
Ujio wa timu hizo unafanywa kwa siri kubwa, lakini MTANZANIA limebaini kuwa watoto wa Jangwani, watawasili kwa kutumia usafiri wa Anga, tofauti na wapinzani wao Simba, ambao wanataraji kuwasili jijini leo kwa usafiri wa maji, huku wakitaraji kulakiwa na mashabiki tayari kuwavaa wapinzani wao Yanga, ambao wana kisasi cha kulipa bao 5-0.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekel Kamwaga alisema watatumia mchezo huo, kuipima vyema Yanga na kujua waanzie wapi kusajili wachezaji watakaokuwa na viwango vya hali ya juu.

Kamwaga alisema mchezo huo utakuwa muhimu sana kwao, ukiachilia mbali masuala ya kuibuka na ushindi kuna mambo muhimu, ambayo kocha wao Patrick Liewig atakuwa na jukumu la kuyaangalia kwa ukaribu.

“Kuna mambo muhimu ambayo kocha atayafanyia kazi siku hiyo, haya yatatusaidia katika mchakato mzima wa usajili wa kikosi chetu kipya cha msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema.

Kamwaga alieleza wameipa nafasi mechi hiyo wakiwa na malengo yao husika, ndiyo maana mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanashinda imefanyika na hilo ndilo wanalowahakikishia mashabiki wao.

Presha kwa mashabiki wa mpira wa miguu nchini imezidi kupanda, huku wengi wao wakisubiri mchezo huo kwa hamu, ambao huvuta hisia za watu wengi hata kwa nchi jirani na Tanzania.

Hali imezidi kuwa imara kwa upande wa matawi ya Yanga, ambapo matawi ya klabu ya Simba ambayo yalikuwa yamegawanyika yameweza kuketi pamoja na kuongeza nguvu, huku kukiwa na tambo za mabango mbalimbali ya kukashifiana.

Halikadhalika tawi la Yanga Ubungo terminal, limeweza kuwa na kikao jana, ambacho wao walikiita cha siri kwa ajili ya kumuua mnyama na kupeleka hamasa uwanjani.
Source: Mtanzania

Next Post Previous Post Home

0 comments:

Post a Comment